Yajue maneno ambayo hupaswi kumwambia mpenzi wako
September 10, 2019
Edit
Migogoro ni jambo la kawaida katika uhusiano wa kimapenzi au ndoa. Na ndiyo maana hata kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi au ndoa si jambo la kushangaza katika jamii. Mahusiano hayavunjiki hivi hivi, zipo sababu.
Ukizifahamu sababu za kuvunjika kwa mahusiano, kama wewe ni mwathirika wa kuvunjika kwa uhusiano utapona haraka na kujifunza kupenda tena. Kwako wewe ambaye uhusiano wako na mwenzako haujavunjika, au labda hata hujawahi kuingia katika uhusiano, unapozifahamu sababu za kuvunjika kwa uhusiano itakusaidia kufahamu jinsi ya kuenenda unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi au hata ndoa, kwa mustakabali mwema wa uhusiano wako na mwenzako.
Kati ya shughuli nzito ambazo huwakumba watu walio katika mahusiano ya kimapenzi au ndoa ni kuhakikisha kuwa mahusiano yao yanakuwa imara. Ni shughuli yenye changamoto nyingi kwani huhitaji uwiano, maana mwanamume na mwanamke wameumbwa tofauti na kila mmoja ana matakwa na matarajio yake.
Sababu za kuvunjika kwa uhusiano zinaweza kuwapo nyingi na kutofautiana kutoka uhusiano huu na ule, lakini zipo kumi ambazo zinaweza kuchukuliwa kuwa kuu. Ukizifahamu utajua jinsi ya kuboresha uhusiano wako wa sasa au baadaye, au kukuweka sawa kisaikolojia kwa ajili ya uhusiano mpya.
Sababu zenyewe ni hizi zifuatazo: -
Kukosekana kwa uaminifu
Kushindwa kutimiza ahadi, kusema uwongo au kufanya usaliti wa kimapenzi ni mambo ambayo humwondolea mtu uaminifu kwa mwenzake. Kwa hakika, kukosekana kwa uaminifu ni sababu kuu ya kuyumba na hata kuvunjika kwa mahusiano yaliyo mengi.
Iwapo kuaminiana kwa msingi kabisa katika uhusiano kutavunjwa mara kwa mara, hasira za mpenzi kwa mwenzake zitalimbikizwa na hamu ya wapenzi/wenza kuendelea kuishi pamoja itapungua. Wapenzi walio katika uhusiano wenye mizizi na afya njema wanaweza kukubaliana kumaliza tofauti zao na kusonga mbele. Kama wataheshimu ahadi na viapo vyao vipya mambo yataendelea.
Kumdanganya mpenzi mara kwa mara, kumsaliti mara kwa mara na kuvunja ahadi zako mara kwa mara huufanya uhusiano kudhoofika na hatimaye nguzo yake muhimu – yaani kuaminiana – kuanguka. Hapo ndipo uhusiano hufika kikomo.
Kutokuwepo kwa uwiano wa madaraka
Katika zama hizi ambapo wanawake wamezifahamu haki zao, kutokuwepo kwa uwiano mzuri katika kutoa maamuzi inaweza kuwa sababu mojawapo ya kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi au hata ndoa.
Inapotokea kuwa mmoja tu ndiye anayetoa maamuzi kuhusiana na shughuli mbalimbali, uchaguzi wa marafiki, masuala ya kifedha, masuala ya nyumbani, likizo na kadhalika, mwingine anaweza kujiona kama vile hana nafasi katika ushirika huu, hivyo kuamua kujitoa.
Katika zama hizi, wanawake wengi wanafundishwa kuwa na hisia za usawa. Iwapo itatokea mmoja wa wanandoa au wapenzi akajihisi kuwa ametengwa katika maamuzi ya msingi yakiwamo yale yanayohusiana na mustakabali wa maisha yake, ni rahisi sana uhusiano kufika kikomo.
Kumtenga mtu na watu wake
Mojawapo ya sababu kuu za kuachana kwa wapenzi ni mmoja kujihisi ametengwa na
marafiki zake aliotoka nao mbali, ndugu, jamaa na wanafamilia wake, kwa kizingizio cha mapenzi.
Mara nyingi, wapenzi hujitenga na watu wao wa karibu kutokana na hofu na kutokujiamini, lakini uhusiano wa aina hii hauwezi kuwa na nguvu na unaweza kujenga mazingira ya kuibuka kwa matatizo mengine ambayo hatimaye yatauua uhusiano.
Wivu uliokithiri
Wivu ni mojawapo ya sababu kuu za kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi au hata ndoa. Wivu wa kupindukia unaweza kusababisha ugomvi ambao nao ni sababu kubwa ya kuachana kwa wapenzi.
Wivu husababishwa zaidi na kutokujiamini kwa mtu. Kwa hiyo, ili kuepuka wivu na kuunusuru uhusiano wa kimapenzi, lazima mtu kwanza ajithamini na kujiamini kuwa anastahili kupendwa na mpenzi wake kama alivyo.