UMRI WA UHUSIANO UHESHIMU!
September 20, 2019
Edit
UKIWA huumizwi na historia ni rahisi sana kufanya maamuzi ya ghafla. Watu wa aina hii wapo sana katika jamii yetu, mara nyingi wamekuwa wepesi wa kuingia na kutoka kwenye uhusiano bila kujali ameishi na mwenzake kwa muda gani. Kinachosababisha hili mara nyingi huwa ni hasira. Watu wenye hasira huwa wanakuwa wepesi sana kufanya maamuzi ya kuachana na wenzi wao lakini ndani ya muda mfupi hujikuta wakijilaumu kwa maamuzi waliyoyafanya.
Ndio maana ninasema historia au umri wa uhusiano inapaswa kuheshimika sana katika uhusiano. Unapokuwa na mwenzi wako, mkatengeneza maisha kwa mwaka au miaka kadhaa, mnakuwa tayari mmetengeneza ‘umoja’ ambao msipouheshimu mtajikuta mkijilaumu. Ndugu zangu, mtu unapokuwa kwenye uhusiano na mwenzi wako kwa kipindi fulani, ni vyema sana kuthamini mchango wa mwenzi wako katika maisha yako.
Ni vyema sana kuheshimu muda mliokaa na mwenzi wako. Heshimu mizizi ya penzi lako, kwani hiyo ndiyo inatengeneza undugu.Mnapokuwa kwenye uhusiano kwa muda mrefu, mnasomana mambo mengi. Mnajuana tabia, kila mtu anamzoea mwenzake kwa mambo mengi.
Mnafika wakati, mazoea yanawafanya umuone mwenzako kama vile sehemu ya maisha yako. Asipokuwepo yeye unakosa furaha, anapokuwepo moyo wako unasuuzika. Unafurahia uwepo wake, unamjua naye anakujua vizuri. Ndio msiri wako, mnashea mambo mengi ambayo pengine huwezi kushea na mtu mwingine yeyote.
Mtu wa namna hiyo ni wa kumheshimu, si mtu wa kumlinganisha na mtu mwingine yeyote ambaye pengine mnakutana leo barabarani. Ni mtu ambaye mnapaswa kwenda naye sawa. Hata ikitokea mmekwaruzana kidogo, usikurupuke tu kuchukua maamuzi ya kumnunia au kusema muachane, jipe muda wa kumtafakari mwenzi wako na baadaye mtasameheana. Usifanye uamuzi wowote wa haraka katika kipindi ambacho mwenzako amekukwaza. Uamuzi huo unaweza kuja kuujutia baadaye. Marafiki zangu maisha ya uhusiano yako hivi, awali mnapoanzisha uhusiano huwa unakuwa peke yako lakini kadiri muda unavyozidi kwenda, penzi linahusisha watu wengi zaidi.
Ndugu, jamaa na marafiki nao kwa namna moja au nyingine wanakuwa sehemu ya uhusiano wenu. Wanashirikiana nanyi katika safari yenu. Wanakuwa na imani na nyinyi, wanakuwa na matarajio na nyinyi, wanawaombea. Hapo ndio utaona umuhimu wa kuheshimu historia ya penzi lenu. Kadiri miaka inavyozidi kwenda, mnawashirikisha watu wa pande mbili na baadaye kufikia kuwa ndugu.
Upande wa mwanamke na upande wa mwanaume unakuwa kitu kimoja, mnakuwa ndugu. Hayo ndio maisha ya uhusiano yanavyobeba dhamana kubwa. Ukumbuke unapochukua uamuzi wa hasira, ukaachana na mwenzi wako ambaye mmedumu muda mrefu ukumbuke pia uamuzi huo unakwenda pia kuwagusa wale wote ambao mlikuwa mmewaunganisha.
Unawagusa wale waliokuwa na matarajio makubwa na nyinyi. Walitamani kuwaona mnafika mbali, walitamani kuona safari yenu inakwenda kuwa na mafanikio na mwisho wa siku mzae watoto na kukuza ukoo. Kwa uzito huo ndio maana ninasema, umri wa uhusiano ni dhamana kubwa, kila mmoja anapaswa kuuheshimu.
Kauli zile za jeuri kwamba; ‘hatukuzalia pamoja’, ‘tumekutana ukubwani’, ‘aniache na maisha yangu’ na nyingine kama hizo ni za kijinga. Utazijutia tu ndani ya muda mfupi, heshimu umri wa penzi lenu, mtaishi miaka mingi na kufurahia mahusiano yenu.