KARAMU YA ABUNUASI
June 24, 2019
Edit
Hapo zamani za kale aliondokea Abunuwasi. Abunuwasi huyo aliishi katika mji mmoja wenye watu kidogo. Katika mji huo Abunuwasi alikuwa mtu maarufu sana kwa sababu alikuwa mcheshi, mchangamfu, na mtu wa masihara sana. Alipenda kucheza na kufurahisha watu. Abunuwasi alijulikana na kila mtu. Siku moja Abunuwasi aliota ndoto. Katika ndoto hiyo aliota kuwa babu yake aliefariki miaka mingi amekuja kumpa ujumbe. Ujumbe huo ulikuwa anamtaka Abunuwasi afanye karamu kubwa. Katika karamu hiyo Abunuwasi alitakiwa achinje ng`ombe mkubwa na kupika wali mwingi. Kisha alitakiwa awatafute vipofu arubaini katika mji ule waje kula chakula hicho. Bahati mbaya yule babu yake hakumwambia Abunuwasi wapi atawapata vipofu hao arubaini. Asubuhi Abunuwasi aliamka na kujiuma kichwa. Alijiuliza maswali mengi kisha akasema;`` Ndoto hii lazima iatakuwa ya kweli. Babu yangu hawezi kuja usingizini akaniambia uongo. Huu ni ukweli. Lazima niifanyie kazi haraka. Sasa nitatafuta mchele na yule ng`ombe wangu mkubwa nitamchinja kwa ajili ya karamu. Sawa!``.
Baada ya hapo Abunuwasi alimaliza. Siku ile Abunuwasi alikwenda madukani kutafuta mchele. Kisha alimchukuwa ng`ombe wake mkubwa na kumuweka tayari kwa ajili ya shughuli. Lakini Abunuwasi alikuwa hajuwi wapi atawapata vipofu arubaini kwa sababu katika mji ule kulikuwa na vipofu wasiozidi watano. Abunuwasi hakukujuwa la kufanya.aliendelea tu na matayarisho ya karamu mpaka alipokamilisha kila kitu. Siku ya karamu ilipofika Abunuwasi alipita mji mzima na kunadi karamu yake. Alikuwa akisema;``Hee! WANANCHI! leo ni leo asie mwana aeleke jiwe. Kutakuwa na karamu ya kukata na mundu nyumbani kwangu leo. Karamu hii ni maalumu kwa watu maalumu. Wahusika wote watapewa kadi za mwaliko. Kila atakaepata kadii ya mwaliko anaombwa kufika mapema bila kuchelewa.`` Abunuwasi alimaliza. Baada ya kutoa tangazo Abunuwasi alikata vipande vidogo vidogo vya karatasi. Vipande hivyo vilikuwa ni kwa ajili ya mualiko. Kisha alichukuwa ngozi ya ng`ombe na kuanza kuiburura mitaani. Kila alipopita watu walimshangaa. Wengine walimuuliza `` Abunuwasi unaburura nini?``. Abunuwasi hakujibu kitu ila alikuwa akimpa kadi ya mwaliko kila alieuliza suali hilo. Baada ya muda kupita karamu ilikuwa tayari kuliwa. Abunuwasi nae alimaliza kutowa kadi zake zote.
Wakati wa kula ulipofika,kila aliepewa kadi ya mwaliko alikuwa amehudhuria. Hapo Abunuwasi aliwakaribisha chakula. Watu walianza kula mpaka wakashiba.Walipomaliza kula Abunuwasi aliwashukuru sana na aliwambia;``Nawashukuru sana nyote mliohudhuria katika karamu hii. Kwani kabla a hapo nilikuwa sijui la kufanya. Nilitakiwa nifanye karamu hii na kuwaalika vipofu wa mji huu waje kula.Kama mnavyojuwa ndugu
zangu mji huu hauna vipofu wengi au pengine wapo lakini hatuwajui.Sasa mimi niliposhindwa nilipita na hii ngozi.Sasa ninafahamu kuwa kila mtu anajuwa kuwa hii ni ngozi au sio?``.Watu waliitikia kwa pamoja ``Hiyo ni ngozi``.Abunuwasi aliendelea;``Sasa nilipoanza kuburura ngozi hii kuna watu waluniuliza; ``Hiyo nini Abunuwasi?``.Mimi sikuwajibu sababu nilijuwa hao walikuwa hawaoni hivyo niliamuwa kuwaalika kama nilivyoelekezwa na babu yangu. Watu wote walishangaa!