FAIDA ZA WAPENDANAO KUWA MARAFIKI
July 09, 2019
Edit
KUTOKANA na mila mbalimbali, baadhi ya watu wamekuwa wakiamini kwamba mwanamke ni daraja la pili. Daraja la kwanza na lenye kuthaminiwa ni mwanaume. Yaani mwanamke hana kauli kwa mwanaume. Anakuwa kama mtumwa fulani hivi.
Mwanaume akiongea, basi ni maelekezo kama vile rais wa nchi anavyotoa maelekezo kwa watu walio chini yake. Hakuna wa kupinga. Akisema sitaki kitu fulani kifanyike, basi ni mpaka atakapotoa maelekezo mengine. Vinginevyo, maelekezo ya awali yatabaki kusimama kama sheria.
Wapo baadhi ya wanawake wanaofurahia aina hii ya uhusiano kwa sababu ya mazoea. Kwamba wamekuzwa hivyo, mwanaume ni mwanaume. Huu ni mfumo ambao watu wengi wamekuwa wakiuishi. Kuna ambao wanakubaliana nao, wengine hawakubaliani nao.
Watu wengi sana wamekuwa wakiishi katika malumbano katika mahusiano yao kutokana na mfumo huu wa maisha. Mwanamke hataki kuishi kama mtumwa, mume anakomaa kuonesha uanaume wake. Hakuna anayekubali kushuka, balaa linaanzia hapo!
Kwa kuliangalia hilo, ndio maana leo nimekuja na mada hii. Japo kila mtu ana staili yake ya kuishi, lakini nataka tu nikupe faida za wapendanao kuwa marafiki tofauti na kuwa kama vile mtu na mfanyakazi wake.
Mnapokuwa marafiki inawasaidia katika suala zima la kufikishiana ujumbe wa kukosoana. Pale unapokosea, ni rahisi kutumia lugha ya kirafiki na kumueleza mwenzako na yeye akaelewa kwamba ameelezwa na rafiki yake jambo zuri.
Hamgombani bali mnaelezana ukweli. Unapokuwa na mwenzi wako halafu mnaishi kama mtu na bosi wake, unatengeneza mazingira kwamba yule ambaye ni bosi awe tishio. Mfanyakazi anakuwa analiona tatizo, unamuudhi lakini anashindwa kukwambia kwa kuwa tu anakuogopa.
Kumbe basi kuondoa hofu hiyo, mkiishi kama marafiki atakueleza chochote kile anachojisikia kwa wakati anaoona unafaa. Anakuwa huru! Hajibanibani. Mnapokuwa marafiki, mtafurahia sana maisha ya uhusiano kwani ule utani pia wakati mwingine una maana kubwa katika mapenzi.
Utani wenye mipaka unakuwepo, unamtania mwenzako na yeye anakutania. Hata mkiwa faragha anaweza kukueleza kile ambacho anaona kinamfanya apate raha. Mkiwa hamko kirafiki, si rahisi sana kukuelezea jambo zuri analotaka kufanyiwa ili afurahi.
Matokeo yake, anabaki nalo moyoni. Anakufa na tai yake shingoni kwa sababu hujamjengea mazingira ya kusema, hujamfanya awe rafiki. Mnapokuwa marafiki, ni rahisi sana kumsoma mwenzako kwamba nini anapenda na nini hapendi.
Mnapoishi kama bosi na mfanyakazi wake, hauwezi kumjua mwenzako kwa undani. Huwezi kujua furaha yake iko wapi. Utabaki unahisihisi tu, ni hatari pia kwa ustawi wa uhusiano wenu kwani kiu hiyo akiishi nayo kwa muda mrefu, akikutana na ushawishi mzito ni rahisi sana kudanganyika.
Faida nyingine ni hata pale mnapojaaliwa kupata watoto, wakiona mnaishi kirafiki nyinyi kama wazazi wao basi ni rahisi na wao kuiga aina hiyo ya maisha. Watawa-shirikisha mambo yao, wakiwa na changamoto yoyote hawawezi kusita kuwaeleza.
ANGALIZO
Pamoja na urafiki wote niliouainisha hapo juu, lakini kitu kikubwa hapo kinachotakiwa ni heshima kuchukua mkondo wake. Kweli muwe marafiki lakini kila mtu amheshimu mwenzake kwa nafasi yake. Mke ajue huyu ni mume wangu na mume vile vile ajue huyu ni mke wangu.
Utani usivuke mipaka ukachanganyika na dharau, mwanamke amheshimu sana mumewe. Mume nae aoneshe upendo zaidi kwa mkewe na maisha mtayaona matamu!