IJUE HATARI YA KUTAKA UPENDWE KWA KUHONGA!
July 09, 2019
Edit
NI wiki nyingine tena tunakutana kupitia safu hii, nikiamini kwamba umzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida. Leo nataka kuzungumzia suala la uhongaji katika uhusiano. Kuhonga ni tabia ambayo imeshamiri sana katika jamii yetu. Kipindi cha nyuma tumezoea kusikia ama kuona wanaume wakiwahonga wanawake, lakini sasa hivi mambo yamebadilika.
Wanawake nao wameingia katika mkumbo wa kuwahonga wanaume ili wakubali kuwa nao kimapenzi tu ama waoane kabisa. Tabia hii imekuwa ikiwatia majaribuni walio wengi, hali ambayo imesababisha baadhi ya watu wenye tamaa za kijinga kushawishika kufanya
ngono na watu ambao katika mazingira ya kawaida wasingeweza kufanya nao. Ni kitu cha kawaida kabisa kumkuta kijana wa kiume mwenye umri mdogo kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mama mtu mzima ambaye angeweza kuwa mama yake. Lakini hafanyi hivyo kwa matakwa yake, bali kwa kushawishiwa na pesa ama vitu vingine vya thamani.
Kuna utata kidogo katika neno hili kuhonga, wapo wanaojiuliza kwamba hivi ninapompatia mpenzi wangu fedha kwa ajili ya matumizi madogomadogo nitakuwa nimemhonga? Katika uhalisia neno kuhonga ni kitendo cha mwanaume kutoa fedha ama zawadi kwa kumpa mwanamke, hasa pale anapomtongoza ili awe mpenzi wake ama mke wake.
Pia katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu neno hilo limetafsiriwa kama “malipo ama zawadi itolewayo ili kupata kile unachohitaji au kutaka jambo f’lani liharakishwe”, kwa maana nyingine ni rushwa.
Maana halisi ya kuhonga itapatikana kutokana na nia ya mwanaume hasa pale anapotoa pesa ama kitu kingine kwenda kwa mwanamke. Kwa mfano kama unatoa pesa kwa ajili ya kumsaidia mpenzi wako ama kumkidhia haja mke wako kutokana na tatizo fulani alilonalo, hapo haiwezi ikachukuliwa kwamba umemhonga.
Lakini kama unatoa kitu ama pesa kutaka kulazimisha ama kumshawishi awe rafiki yako, mpenzi wako, mke wako ama kwa kutaka kufanya naye mapenzi, hapo itachukuliwa kwamba umehonga. Kikubwa unachotakiwa kujua ni kwamba, hakuna uhusiano wowote baina ya mapenzi na pesa. Ndio maana mapenzi yanaweza kuwepo hata pale pesa inapokosekana.
Kwa kuthibitisha hilo; wengi wanaopata penzi kwa njia ya kuhonga, mapenzi yao hayadumu kutokana na mmoja kati ya wawili hao kushawishika kutengeneza uhusiano kutokana na pesa ama kitu kingine. Utafiti unaonesha kwamba, kwa wanaume walio wengi kuhonga ni sehemu ya maisha yao licha ya kwamba ni katika viwango tofauti.
Hakuna mwanaume asiyehonga, ukiachilia mbali wale ambao ni waumini kikwelikweli ambao nao sina uhakika kama hawaingia katika kundi la wahongaji kwa maana halisi ya kuhonga.
Licha ya kwamba wapo pia baadhi ya wanawake ambao wana tabia ya kuhonga wanaume ili wawapende, kasi imeonekana kuwepo kwa wanaume ambapo hulazimika kutoa mamilioni ya pesa, magari, simu za mikononi, na vitu vingine vya thamani kwa mabinti ili tu waweze kuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Kimsingi niseme tu kwamba, katika uhusiano wa kweli baina ya wawili waliotokea kupendana, suala la kuhongana hakuna. Usimpe mpenzi wako pesa ili kumlainisha akufanyie jambo fulani kwani ipo siku utakuwa huna pesa na unataka akufanyie, hapo ndipo mnaweza kuachana.
Msaidie pale atakapohitaji msaada wako, kama nilivyowahi kusema huko nyuma kwamba; hutakiwi kuwa m’bahili kwa mwenza wako, kwani wewe ni yeye na yeye ni wewe. Na pia nikutahadharishe tu kwamba, endapo utalazimisha mtu akupende kwa sababu ya pesa au mali zako, penzi haliwezi kudumu na kuachana kuko waziwazi.