Athari ya kitambi kiafya
July 12, 2019
Edit
Kitambi ni hali ya kiafya ya mtu mnene ambapo mafuta ya ziada mwilini huongezeka eneo la tumbo kwa kiasi kikubwa.
Mtu akiwa na kitambi anapata athari kubwa ikiwamo kupungua kwa umri. Katika karne hii, hili ni mojawapo ya tatizo kubwa la kiafya duniani. Hata hivyo, tatizo la kitambi kiafya linarekebishika.
Katika mawazo ya kizamani na hata sasa katika baadhi ya nchi mtu akiwa na kitambi anaonekana ni tajiri.
Tatizo la unene na vitambi litazidi kuongezeka ikiwa serikali, hususan wananchi wenyewe hawatachukua hatua za dharura na mipango madhubuti kulikabili.
Vitambi hupunguza maisha ya watu wenye hali hiyo ya afya, hivyo kusababisha upotevu wa rasilimali watu.
Ili kuepukana na athari hiyo watu wahakikishe wanabadili namna wanavyoishi na milo yao. Wengi wana muda mchache sana wa kutayarisha vyakula visivyo na mafuta mengi majumbani mwao, hivyo wanakula nje zaidi, yaani kwenye hoteli na migahawa na matokeo yake ni kuwa na vitambi.
Kuna wengi wanatambua athari za tatizo la unene na vitambi, lakini hawafanyi chochote kulirekebisha, hii inatokana na ukweli kwamba idadi kubwa ya watu hawajui maana halisi ya kuwa na afya njema.
Watu wengi, hasa vijana wamekuzwa kwa kula chipsi, mikate na vyakula vya sukari na si mbogamboga na matunda.
Ukweli ni kwamba watu wengi hawafanyi mazoezi ya kutosha kama ilivyokuwa zamani hivyo, watu wenye vitambi wanaongezeka kila sehemu.
Kwa ujumla, umri wa mtu mnene mwenye kitambi huwa pungufu kwa miaka 8 had 10 ukilinganisha na mtu mwenye umbo la kawaida.
MAGONJWA
Hii inatokana na ukweli kwamba uzito wa mtu husababisha magonjwa ya moyo, aina fulani ya kisukari, magonjwa ambayo huua mamilioni ya watu duniani kote. Kifupi ni kuwa ukiwa na mafuta mengi mno utakuwa kwenye hatari ya kukumbwa na magonjwa kama ya kupanda kwa presha, magonjwa ya moyo, kansa. Kuongeza uzito au kunenepa kunasababisha mwili ushindwe kupata sehemu ya kutosha ya kuhifadhi mafuta na hivyo kuanza kuyatunza mafuta hayo kwenye sehemu za ndani ya mwili, kuuzunguka moyo na ndipo matatizo yanapoanza.
USHAURI
Kila mtu aepuke kula vyakula vyenye mafuta mengi na kutokula chakula kupindukia na ule unaposikia njaa, kutotia mafuta mengi kwenye chakula na kutotumia sukari nyingi.
Kila mtu anatakiwa kufanya mazoezi ya kukimbia, kutembea au kuogelea angalau kwa nusu saa kila siku.
Watu wanashauriwa kuacha kutumia vyakula vya kopo na hasa vile vyenye gesi nyingi. Wale ambao ni wanene kupita kiasi waonane na daktari kwa ushauri wa kitaalamu.