KUNA WANAOAMINI NDUMBA KWENYE MAPENZI, USIWAPUUZE! - RAHA ZA KITANDANI

KUNA WANAOAMINI NDUMBA KWENYE MAPENZI, USIWAPUUZE!


MUNGU ni mwema, Jumatano nyingine ametujaalia tunakutana katika jamvi letu la ulimwengu wa mahaba. Kama ilivyo ada, hapa tunapanuana mawazo juu ya suala zima la maisha ya mahusiano kwa ujumla.

Uhusiano wowote ule lazima uwe na misingi. Tunaelekezana mawili matatu ambayo yanaweza kusaidia safari yako ya maisha ya uhusiano iwe nzuri. Utoke kwenye uhusiano usioleweka, kwenda katika uhusiano ambao unaeleweka na hatimaye uweze kuishi maisha ya ndoa.

Ndugu zangu, kupata mume au mke mwema si kazi rahisi. Inahitaji maandalizi, inahitaji kujitengeneza na kumtengeneza huyo unayemtaka awe mwenzi wako wa maisha. Kwenye eneo la kujitengeneza lazima ujitambue, ujue wewe ni nani na unataka kuwa na mtu wa aina gani.

Utakapompata, unapaswa pia kutambua kwamba kuna vitu utapaswa kujifunza kutoka kwake na vingine yeye atajifunza kutoka kwako. Mtashirikiana katika kila jambo. Kwenye safari ya mahusiano, mnakutana ukubwani. Kila mtu anakuwa amepita njia zake, mwisho wa siku mnaamua kuwa pamoja, hivyo lazima mchukuliane tabia.


Yawezekana mwenzako akawa amekulia kwenye malezi yasiyokuwa ya maadili, unapaswa kumbadilisha taratibu. Anaweza kuwa na tabia fulanifulani ambazo pengine kwa namna  zinaweza kuwa si nzuri, hivyo mnapaswa kuelekezana.Yawezekana mwenzako akawa amekulia kwenye familia ambayo inaamini mambo ya kishirikina, inayapa kipaumbele kuliko kitu kingine chochote, hivyo ni jukumu lako pia kumbadilisha.

Zipo familia ambazo kitu kidogo tu, kwa mganga. Hawaamini kwamba Mungu yupo na atosha kuwalinda na mambo yote ya kishirikina. Hivyo, mtu wa aina hiyo yakupasa kutumia nguvu za ziada kumbadilisha ili aweze kuelewa kwamba imani hizo hazifai. Mtu ambaye tangu anakua ameishi kwenye mazingira hayo, si kazi ndogo kumbadilisha. Inahitaji nguvu ya ziada na msaada wa Mungu ili uweze kufanikiwa kumfanya aamini katika Mungu.

Kwenye maisha ya uhusiano, cheni ya matukio ya kishirikina ina mianya mingi, yawezekana wewe ukawa huamini na mwenzi wako haamini lakini mpenzi wako wa zamani akawa anaamini. Yawezekana ukiwa kwenye uhusiano mpya, yule uliyekuwa naye awali akawa bize na masuala ya kishirikina, hajaridhika akawa kutwa anafanya ‘manuva’ yake kukuharibia ulipo.
Image result for COUPLES
Ukiwa haupo imara katika misingi ya dini, unaweza kukuta umetetereka. Unayumbishwa na mambo mbalimbali ambayo yanaweza kukutokea au kumtokea mwenzi wako mpya uliyenaye. Unachotakiwa kufanya, kuwa na imani thabiti. Kusimama na mwenzi wako, amini kwamba hakuna ushirikina ambao unaweza kuizidi nguvu ya Mungu.

Unapotokea umekutana na changamoto ya aina yoyote katika safari yako na mwenzi wako, kwa imani yenu mnapaswa kumuomba Mungu awasaidie. Mmuombe Mungu awaondelee jaribu hilo. Mmuombe yeye awasimamie katika safari yenu. Muombe ulinzi wake katika safari yenu ili asiwepo mtu wa kuwaharibia.

Wenye roho mbaya, wenye jicho baya, wivu na mambo mengine yanayofanana na hayo, washindwe kuwafanyia jambo lolote, wawaone tu mkiishi vizuri mkifurahia maisha ya urafiki, uchumba na hata ndoa. Sema amina!