SIO KILA MPENZI ANAWEZA KUWA MUME, MKE
July 10, 2019
Edit
MUNGU ni mwema, Jumamosi nyingine tunakutana katika uwanja wetu wa mahaba. Hapa tunapata kujifunza, kujadiliana na kuweza kupeana ushauri wa maswala ya mahusiano. Ulimwengu wa sasa una changamoto nyingi. Ni vigumu sana kumpata mtu sahihi maana kila mtu ana maumivu yake. Watu wengi wamejeruhiwa, wanajuta kupenda kutokana na waliyoyapitia. Lakini nikutie moyo tu wewe unayesoma sasa, mume au mkeo yupo.
Ni suala la muda tu, lakini ipo siku utakutana naye. Siku hiyo hutaamini kwamba kweli na mimi ninaitwa mke au mume wa fulani maana ulishakata tamaa. Ulikutana na walaghai wa kila aina, wenye maneno matamu kumbe hawana mapenzi ya dhati.
Upande wao wa pili ni hatari. Mtu unaishi na mwenzako, unamuamini na kumpa moyo wako wote mwisho wa siku anakuja kukutenda. Anakuacha kwenye kipindi ambacho wewe hukujiandaa. Ulikuwa na mategemeo makubwa na yeye, akili yako iliwaza mbali.
Marafiki zangu mnaosoma hapa, niwaambie tu kwamba msikate tamaa. Kikubwa ambacho kila mmoja wetu anatakiwa kufahamu ni kwamba, maisha ya uhusiano yana siri kubwa ambayo wakati mwingine kuielewa huwa ni vigumu.
Si kila anayekuita baby, sweet, honey na majina mengine kama hayo anaweza kuja kuwa mume au mke wako. Wapo wengi ambao utakutana nao katika maisha ya uhusiano kama sehemu ya kukujenga na kukuimarisha katika safari yako ya ndoa.
Wapo watu watakufuata tu kwa ajili kukufundisha kwamba katika mahusiano kuna matapeli wa mapenzi. Kuna watu ambao hawana huruma. Kuna watu ambao hawathamini hisia za watu wengine. Kuna watu ambao ni hodari kwa kuumiza mioyo ya wengine.
Kweli unaweza kujikuta umezama penzini, ukashindwa kumbaini mapema uliyenaye ni tapeli. Lakini atakapokuja kujidhihirisha huko mbele ya safari, na ukawa umejitahidi kumfanya awe wako, na ikashindikana basi muache aende.Umeishi naye kwa mwaka mmoja, miaka miwili au hata mitatu, mwenzako akaanza kuleta za kuleta, pambana kumweka kwenye himaya yako.
Pigania penzi lako kama unaweza na itakaposhindikana, kaa pembeni. Ni vigumu kukubaliana na matokeo lakini ifike mahali ukubali yaishe. Kama kupigania penzi lako umepigana sana, umefanya kila linalowezekana kurejesha uhusiano wako lakini imeshindikana, basi huna budi kumshukuru Mungu kwa yaliyotokea.
Hakupangwa kuwa mume au mkeo wako. Alikuwa ni mtu wa kupita. Alikuwa sehemu ya fundisho tu kwako na kujua watu wa aina hiyo walivyo. Anakupa somo hata baadaye utakapokutana na mtu mwingine, uwe makini.
Usikurupuke kuanzisha uhusiano mpya. Jifunze kwanza watu sahihi wakoje. Wana sifa zipi? Amini kwamba maisha lazima yaendelee. Acha kuwa na mawazo, ifurahishe nafsi yako kwa kujichanganya na mambo mengine ya kimaisha. Ipo siku yako, utampata mtu ambaye hatakawia kutoka kwenye urafiki, uchumba na hata kufikia kuwa mke au mumeo.
Hutaamini. Mambo yatajipa tu haraka au taratibu lakini kikubwa ni kwamba wewe utasahau yote uliyopitia. Yatabaki historia, ili ufikie kwenye kilele lazima ukutane na changamoto, hivyo usiumizwe na changamoto.
Ziache zije huku wewe ukiamini kwamba zinapita na mume au mke wa maisha yako yupo mahali, anangoja siku na saa tu itimie ili muweze kukutana!