JINSI YA KUWAEPUKA WALAGHAI WA MAPENZI
July 10, 2019
Edit
MAISHA yanaenda kasi sana huku suala la ndoa likiwa ni kipaumbele cha kwanza na kigumu kwa wanawake. Wengi hujikuta wakichanganyikiwa pindi tu wanapotangaziwa ndoa. Mwanamke akiambiwa nakuoa, akili yote inamruka.
Hana muda wa kuhoji mara mbili, cha muhimu ni kusikia tu ile kauli ya ‘nitakuoa’. Hiyo kwake ni kauli pekee inayomfanya atembee kifua mbele. Anakukabidhi moyo wake jumlajumla, hana muda wa kupoteza, anaingia mzimamzima.
Matokeo yake, kizazi cha sasa kimejikuta kwenye janga hili kubwa. Wanawake wengi wanalia. Wanalainisha uhusiano na kuzama pale tu wanapopewa kauli ya matumaini kwamba wataolewa. Hawana muda wa kuchunguza.
Wengi wamejikuta kwenye mikono ya matapeli wa mapenzi. Wanaingia kwenye uhusiano, wanaume wakishapata wanachotaka basi biashara inakuwa imeishia hapo. Mwanamke anabaki njia panda, hajui nini cha kufanya.
Aliyekuwa naye kwenye uhusiano alimpenda sana. Aliwekeza akili zake zote kwake. Moyo wake ulikufa, ulioza. Dunia anaiona chungu maana yule aliyedhani ni mwenza wake wa maisha, kumbe ni tapeli mkubwa. Anamuacha bila huruma.
Bahati mbaya sana, anaposema ajaribu kuanzisha uhusiano mwingine pia anakumbana na majanga yaleyale. Kajamaa kanajifanya kanampenda, kanamjali kumbe kanafiki tu. Ndani ya muda mfupi kanamuacha solemba na matokeo yake mwanamke analia tu.
Anakuwa ni mtu wa kumwaga machozi kila uchwao. Kila akikumbuka mapito yake, anajiona kama vile ni mkosaji. Anajiona kama Mungu hampendi, anawapendelea wenzake wengine ambao wako kwenye mahusiano mazuri.
Anajiuliza kwa nini yeye? Kwa nini wenzake wengine wanayafurahia maisha ya uhusiano na wapenzi wao lakini kwake suala la mahusiano ni kama kaa la moto. Kila siku mtu wa kulia, akipata furaha ni ya muda mfupi, anarudi kwenye majanga yaleyale.
JIFUNZE!
Si kila anayekwambia anakuoa basi kweli ni muoaji. Wanaume wengi siku hizi hutumia kigezo hicho kama sababu ya kuwahadaa wanawake. Unapaswa kuwa makini. Mwanaume akikuambia anakupenda na anataka kukuoa, mchunguze kwanza.
Kabla ya kuruhusu moyo wako kumpenda, hakikisha kwanza umejiridhisha. Huyo anayekwambia anakuhitaji, atakuoa ni kweli anamaanisha. Je ana tabia njema? Fanya uchunguzi kwanza. Umjue vizuri, ametokea wapi, asili yake ikoje na ikiwezekana familia yake kwa ujumla.
Umjue kama ana hofu ya Mungu. Asikwambie mtu, hakuna sababu ya kuharakia ndoa. Unaweza kuharakia na mwisho wa siku usidumu. Unaweza kuingia kwenye ndoa na jambazi. Unaweza kuingia kwenye ndoa na mtu katili ambaye yeye muda wote anawaza kuua tu.
Unaweza kuingia na mtu kwenye ndoa yeye muda wote anawaza ugomvi. Muda wote ni kama mikono inamuwasha. Mtu wa aina hiyo, mnaweza kuingia naye kwenye matatizo makubwa na ndoa yenyewe ukaiona chungu.
Mchunguze mtu taratibu. Jipe muda. Mshirikishe Mungu katika safari yako. Umtambue mwenzi wako ni sahihi au la. Ukimtumaini Mungu, hakika utapata jibu lililo sahihi. Hakika utampata mwenza ambaye ndiyo chaguo lako.
Ipo siku tu, usiumie. Usiishi kinyonge, muombe yeye, mtumaini Mungu kamwe hawahi wala hachelewi. Utapata majibu kwa wakati wako ukifika. Mchunguze mtu hata kwa mwaka mmoja au hata miwili ndipo ukijiridhisha, mpende!
Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo hapahapa. Waweza pia kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii, Instagram na Facebook natumia jina la Erick Evarist, Twitter ni ENangale. UNAWEZA KUINGIA NA MTU KWENYE NDOA YEYE MUDA WOTE ANAWAZA UGOMVI. MUDA WOTE NI KAMA MIKONO INAMUWASHA. MTU…