USISEME HUNA BAHATI, UMEJIKAGUA VYA KUTOSHA?
June 30, 2019
Edit
DUNIA ya sasa imejaa sarakasi nyingi sana katika masuala ya mahusiano. Huyu anampenda yule, mwenzake hampendi. Anayemkataa mwenzake naye anampenda mtu mwingine ambaye naye huyo mtu hampendi vilevile basi ili mradi tu mambo yanakwenda ndivyo sivyo. Kila mtu ana maumivu yake. Kuna ambao wanalia kuachwa, kuna wengine ni mahodari wa kuacha basi ni fujo tu. Kila mtu ukikutana naye na akakusimulia maisha yake ya mahusiano yanaweza kujaza hata kitabu. Mlolongo wa matukio unaweza kuwa mrefu ambao unaweza kuhuzunisha na hata kukufanya ukasirike na uone mapenzi hayana maana.
Pamoja na mlolongo wa matukio hayo lakini nikutie moyo tu kwamba bado inawezekana. Nafasi ipo ya wewe kuingia kwenye uhusiano na ukadumu na mwenzi wako. Historia isikutese, isikuumize maana kila kitu kinakuja katika muda muafaka.
Muda uliopoteza katika mahusiano yaliyotangulia ni sehemu ya njia ya kukuimarisha. Kukufanya uwe ngangari kukabiliana na uhusiano wako sahihi. Usikate tamaa, amini kwamba ipo siku tu na wewe utaishi na mwenzi wako sahihi. Marafiki zangu, siku zote nimekuwa nikisisitiza katika makala zangu mbalimbali kwamba hakuna jambo kubwa na la muhimu kama vile wewe mwenye kujifanyia tathimini kabla ya kuingia kwenye uhusiano hususan wa kimapenzi.
Jikague kupitia aina ya maisha unayoishi, je unafaa kuwa mume au mke wa mtu? Hauna tabia mbayambaya? Japo ni ngumu kujifanyia tathimini lakini niamini mimi, kila mwanadamu ana ‘sensa’ ya kawaida kabisa ya kuweza kujua mazuri na mabaya.
Mathalan, mtu anajua kabisa kwamba tabia yangu ya kupenda wanawake wengi tofauti ni mbaya lakini anashindwa tu kuiacha. Mtu anajijua kabisa ana kisirani lakini hawezi kuacha. Mwingine anajijua kabisa ni mlevi lakini hataki tu kuacha. Nasema hivi nikiwa na maana, mfano wewe ni mlevi na unajua fika kwamba pombe ina madhara katika maisha yako, kwa nini uendelee kuinywa? Kama unashindwa kujidhibiti katika ulevi, kwa nini ushindwe kuacha?
Nasema hivyo kwa sababu kuna wakati mtu huwa unajikagua na kuona kabisa ulevi unakuangusha lakini bado unataka kumpata mwenza sahihi ambaye pengine ni mtu asiyekunywa pombe mathalan mlokole. Hivyo basi kabla ya kumtafuta mwenzi wako unapaswa kujikagua.
Jikague kwanza wewe ni nani? Kipi kinakukwamisha pindi unapokuwa kwenye uhusiano? Ukijikagua bila ya kujipendelea bila shaka utakijua kiini cha matatizo yako katika mahusiano. Ukishakijua unapaswa kukifanyia kazi.
Kama unajua tatizo lako ni kipato duni, tafuta fedha kwa nguvu. Kama tatizo lako ni ulevi, umalaya basi ni vyema ukajisahihisha ili uweze kuishi vizuri katika mahusiano. Unaweza kukuta unajilaumu kwamba pengine una mikosi kumbe huna mkosi wowote, hujajikagua.
Jikosoe, jiambie kwamba suala hili kwangu ni kikwazo hivyo nifanye kila linalowezekana kujisahihisha. Ukishajisahihisha wewe itakupa nafasi nzuri ya kumsahihisha mwenzi wako ambaye atakuwa na tatizo kama la kwako au matatizo mengine.
Ukishakuwa vizuri wewe, itakuwa rahisi kumfanya mwenzi wako awe mzuri. Ndege wapendanao ndio wanaoruka pamoja hivyo mkiwa tofauti msitegemee kwenda sawa. Ukiwa na tabia chafu usitegemee kupata mtu sahihi, utaishia kupata watu wanaofanana na wewe na kamwe hamtadumu!
Fanya yaliyo sahihi ili uweze kumpata mtu sahihi. Huwezi kumpata mtu sahihi na mkadumu kama wewe mwenyewe sio mtu sahihi, badilika!