HADITHI: Maisha ya ndoa - RAHA ZA KITANDANI

HADITHI: Maisha ya ndoa

Baada ya kumaliza sherehe ya ndoa yao, mama wa bibi harusi alimpa binti yake notebook yenye namba mpya ya Akaunti ya benki ikiwa na kiasi cha shilingi laki tatu.
Mama alimwambia hivi, "binti yangu, chukua hii notebook, itunze kama kitu cha kuandikia rekodi katika maisha yako ya ndoa, chochote cha kufurahisha kitakachotokea katika maisha yako haya mapya na mumeo, weka pesa katika akaunti hii na uandike katika notebook juu ya hiyo furaha yako/yenu.


Matukio ya kufurahisha yatakavyotamalaki katika ndoa yenu yakizidi nawewe ndio uzidi kuweka kiwango zaidi cha fedha utakayokuwa nayo kama akiba bila kusahau kuweka rekodi ya hiyo furaha.
Fanya hili na mumeo ili mtakapotizama baada ya miaka kadhaa mtambue ni kwa kiasi gani mlikuwa na furaha katika ndoa yenu.
Binti alipokea hayo maelekeza na akaenda kumueleza na mumewe. Wanandoa waliona kwamba ni jambo jema kwao na vilevile ni njia mojawapo ya utunzaji wa fedha.
Wakawa wakisubiri tu panapofuraha kati yao ili wewekeze hizo pesa.
Hivi ndivyo ile notebook ilisomeka baada ya kipindi kirefu kidogo cha ndoa yao;
7 February- Tsh 100,000 - birthday ya kwanza ya mume wangu tukiwa katika ndoa
1 March- Tsh 110,000- Mume wangu amepandishwa cheo kazini.
20 March- Tsh 120,000 - Tumeenda likizo Zanzibar.
29 April - Tsh 125,000 - Ujauzito wa kwanza.
5 september - Tsh 130,000 Mume wangu amenifulia nguo zangu zote chafu baada ya mimi kuwa hoi ujauzito ukinisumbua.
8 October - Nimemnunulia mume wangu saa aipendayo, amefurahi sana….
List ilikuwa ndefu sana……..
Hata hivyo miaka ilisonga na wanandoa wakaanza ugomvi na mabishano baina yao. Wakawa hawana ukaribu tena na kila mmoja akawa anajutia ndoa yao, hakukuwa na mapenzi tena kati yao.
Siku moja binti alimpigia mama yake simu. "mama siwezi kuvumilia tena, tumeamua tuachane, najuta kwanini nilikubali kuolewa na huyu mwanamume!" Binti alisikika na mama yake akiongea.
Mama yake akamjibu, "Mwanangu siungi mkono jambo unalotaka kufanya ila siyo kesi kubwa fanya kile ambacho moyo wako umeamua ila kabla ya hapo fanya kitu kimoja. Unakumbuka ile notebook niliyokupa? Nenda katoe pesa zote benki na utumie na mumeo kabla hamjaachana.!
Hivyo yule binti alienda benki, na wakati amesimama kwenye foleni alichukua ile notebook na kuanza kusoma matukio ya furaha na faraja waliyoyapitia yeye na mumewe.
Jinsi alivyokuwa akizidi kuyasoma yale matukio ndipo kumbukumbu za furaha na mapenzi vilizidi kuujaza moyo wake, na machozi yakiwa yanamtoka, akaghairisha na kurudi nyumbani.
Alipofika nyumbani alimkabidhi mumewe ile notebook na kumwambia aende akatoe zile pesa wagawane kabla hawajatalikiana.
Nae alipoenda benki akiwa katika foleni akisoma ile notebook nae alipatwa na hali ile ile, aliamua asitoe zile pesa. Na akarudi nyumbani.
Akiwa na mkewe, waliamua kufanya mahesabu wajue ni kiasi gani kilichokuwemo katika akaunti, walipofanya majumuisho ya matukio yote ya furaha waliyoyarekodi walijikuta wakiwa na shilingi milioni tatu na laki tano.
Kwa mshangao mume akamwambia kwamba leo ndio nimegundua ni kwa thamani gani ninakupenda, ni kwa kiasi gani umeleta furaha kwenye maisha yangu, na ni kwa kiasi gani nilivyo mpumbavu kukata tamaa juu yako na kuzitupa kumbukumbu zote nzuri tulizoshea pamoja.
Wakakumbatiana kwa upendo na mapenzi yao yakachanua upya, wakaandika tena lile tukio la kuwaunganisha pamoja na kwenda kuweka pesa benki.
Na notebook wakaitunza tena katika sehemu iliyo salama kwa ajili ya kuendelea kuandika rekodi.
___
Ndoa sio mchezo wa kuigiza, sio kitu rahisi ila ni nzuri. Mtabishana, Mtagombana na kununiana ila ni kawaida kwa sababu kila mmoja ametoka katika familia zenye historia tofauti.
Usitegemee kila utakachozungumza kitakubaliwa na mwenzako moja kwa moja bila kutoa maoni yake. Ila kabla ya kukata tamaa katika ndoa fikiria nyakati nzuri kabisa mlizoshea pamoja na kuwaweka karibu.