PESA INAPOGEUKA KIUNGANISHI KWENYE MAPENZI, HESABU MAUMIVU
April 15, 2019
Edit
IJUMAA imewadia, karibu msomaji wangu kwenye uwanja huu na kama kawaida, mada ya leo ni kama inavyojieleza hapo juu. Uhusiano wa kimapenzi una changamoto nyingi, ukiachana na mambo ya usaliti na kuumizana mioyo, suala la pesa ni tatizo jingine linalowasumbua wengi.
Ukizungumza na wanaume wengi, watakueleza wazi kwamba wapo kwenye uhusiano na wanawake ambao wanajua kabisa kwamba hawawapendi bali wanafuata pesa kwao. Yaani haishi na wewe kwa sababu upo moyoni mwake, la hasha! Anaishi na wewe kwa sababu anajua atanufaika kiuchumi.
Kibaya zaidi, siku hizi upepo umebadilika, si wanawake tu wanaofuata pesa kwenye mapenzi, wapo wanaume ambao wanapenda mteremko, anakuwa na uhusiano na mwanamke fulani, hata kama amemzidi sana umri, si kwa sababu anampenda bali kwa sababu ana pesa, ana nyumba, magari, kazi nzuri na kwenye kutoa pesa, hana tatizo. Msomaji wangu utakuwa shahidi wa hili kwamba katika siku za hivi karibuni, mapenzi yamekuwa si kutoka moyoni tena, bali kutoka mfukoni! Toa pesa upate mapenzi.
Kwa kawaida, penzi la namna hii, haliwezi kuwa la kudumu mpaka pale tu, pesa au utajiri utakapokuwa wa kudumu, kitu ambacho hakiwezekani. Kama wewe ni mwanaume, unaishi na mwanamke ambaye anatazama zaidi pesa kuliko utu na mapenzi, siku pesa zitakapokauka, atakubadilikia tu.
Siku utakapofukuzwa kazi, siku utakapofilisika kibiashara au utakapopata maradhi yatakayokuweka kitandani muda mrefu, utaanza kuona rangi yake halisi. Atabadilika kitabia, hatazijali tena hisia zako, hatokuheshimu, atakusaliti na kukuumiza moyo wako mpaka utajuta kuzaliwa.
Ndiyo! Si kiunganishi cha mapenzi yenu hakipo tena? Atakupendaje wakati hauna kitu na yeye alifuata pesa kwako?
Jambo la msingi, ni muhimu kumjua mtu ambaye yupo kwako kimaslahi mapema kwa sababu ukimchekea, ni kama kufuga nyoka mdogo ndani ya nyumba yako, ipo siku atakung’ata na kukuua hata kama kila siku ulikuwa ukimlisha unga. Mtihani unaweza kuwa hapo, kwamba utamjuaje huyo uliyenaye kama kweli anakupenda na hafuati pesa kwako? Utajuaje kama anakupenda kwa dhati na hayupo na wewe kimaslahi?
Zipo mbinu nyingi za kumgundua mtu wa namna hiyo na njia nyepesi lakini yenye changamoto kubwa, ni kumpitisha kwenye wakati mgumu. Wahenga wanasema, nahodha mahiri hapimwi kwenye bahari iliyotulia. Mpitishe katika kipindi ambacho yale maisha aliyoyazoea kutoka kwako, hayapo tena. kama ulizoea kumpa fedha za kuchezea, kila anachokitaka unampa, hebu badilisha mchezo.
Hatari ya jaribio hili, ni kwamba kama hakuwa anakupenda kwa dhati, haraka sana ataanza kuonyesha rangiyake halisi, mwingine anaweza hata kukuumiza moyo wako kwa kukusaliti kimapenzi kwa kutoka na watu wenye fedha kwa sababu wewe humpi tena pesa.
Inapotokea hali kama hii, hata kama ulikuwa unampenda kwa kiasi gani, elewa kwamba mwenzako yupo kwako kimaslahi, siku pesa zikikata, atakubadilikia mpaka utashangaa. Ukishaujua ukweli, hata kama utaamua kuendelea kuwa naye, utakuwa umeshajua mtu unayeishi naye ni wa aina gani.
Hakuna mapenzi yanayounganishwa na pesa yanayoweza kudumu, mapenzi lazima yaanze halafu pesa iwe matokeo!