MAMBO MUHIMU AMBAYO MWANAUME HUITAJI KUTOKA KWA MKEWE - RAHA ZA KITANDANI

MAMBO MUHIMU AMBAYO MWANAUME HUITAJI KUTOKA KWA MKEWE


NI matumaini yangu kuwa umzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida. Wiki iliyopita utakumbuka niliishia kuzungumzia suala la busara. Nikasema mwanamke anaweza kuwa chanzo cha furaha kwa mumewe endapo atatumia busara kwa kiwango kinachotakiwa.

Kwa kifupi wanaume wanahitaji sana busara ya mwanamke na kama mwanamke ukiweza kuwa na busara katika kumtatulia matatizo yake hata kwa kumpa mawazo yako na kumpa moyo, ataona umuhimu wako na wakati mwingine kukushirikisha kila afanyalo kabla ya kulifanya hasa baada ya kuona anaishi na mwanamke mwenye busara.

2. Kujali
Imezoeleka kuwa mwanaume ni kichwa cha nyumba na yeye ndiye muwezeshaji wa kila kitu katika familia, hilo ni sawa na halina ubaya wowote, lakini kuna baadhi ya wanawake wanakosa busara ya kawaida kwa kufuja mali za mumewe kisa eti ameolewa.
Mjali mumeo bwana, mume wako anahitaji ujali mali zake na pesa zake kwa ujumla. Kuna baadhi ya wanawake hutumia pesa hovyo kwa matumizi ya chakula na mahitaji mengine ya familia kwa kisingizio kuwa ni wajibu wa mwanaume kufanya kila kitu katika familia.
Maisha siku hizi yamekuwa magumu, mwanaume anapenda kuwa na mwanamke ambaye anajua bajeti vizuri ili awe na uhakika kuwa hata kama siku akiwa hana fedha za kutosha utaweza kutumia kiasi kidogo atakachokupatia. 
Siku hizi wanawake wengi ambao wameolewa nao hufanya kazi kwa minajili ya kujiongezea kipato, sasa kuna baadhi ya wanawake akipokea mshahara wake ni siri yake na hahitaji hata mumewe afahamu kuwa anapata kiasi gani. 
Wanawake wa aina hiyo mishahara yao huishia kununua vipodozi na nguo mbalimbali ili waweze kwenda na wakati huku wakisahau kabisa wajibu wao katika kuwasaidia waume zao.
Huo siyo ustaarabu, unapokuwa unafanya kazi na mumeo pia anafanya kazi ni wajibu wenu kusaidiana kwa kila hali, unapopata mshahara wako ni vyema ukamshirikisha mumeo ili muweze kujua namna mtakavyotumia na siyo kubaki na mshahara wako wote bila ya kumshirikisha mumeo.
Elewa kitu kimoja maisha ya siku hizi ni kusaidiana, hivyo ni wajibu wako wewe mwanamke kumsaidia mumeo kifedha kama unafanya kazi.