MAMBO YANAYOUMIZA WENGI KATIKA UHUSIANO - RAHA ZA KITANDANI

MAMBO YANAYOUMIZA WENGI KATIKA UHUSIANO

KUNA mambo mengi ambayo husababisha wenye uhusiano kuumia roho zao. Leo tuyayaeleza mambo hayo kama ifuatavyo:
KUFICHA MAMBO
Kuna jambo hata ukijaribu kulificha, ukweli wake utajulikana tu hususan kama utakuwa na mahusiano ya muda mrefu na mtu husika. Jambo hilo ni kiukweli, kama unampenda kwa dhati mwenza wako, hutakiwa kumficha jambo, liwe baya au zuri. Mpenzi wako akiwa makini akagundua kuwa kuna jambo umemfika, atakosa uaminifu kwako na ataumia rohoni.
Ukweli ni kwamba ukiwa humfichi jambo mpenzi wako, atakujali na kutokana na matendo yako hususan vile unavyojali hisia zake, usikivu wako kwake, heshima yako kwake, na unavyojali ni dhahiri upendo utadumu na utadhihirisha kudumu kwa uhusiano wenu.
FEDHA
Hata kama mtajitahidi kupuuzia umuhimu wa fedha katika uhusiano wenu, lakini fedha itabaki kuwa mhimili mkubwa wa uhusiano wenu. Hata kama nyote mnaingiza kipato, kuna changamoto mtazipata kama vile kupanga kwa pamoja jinsi ya kutumia fedha zenu, au kujieleza kuhusu matumizi fulani ambayo mwenzi wako atahoji. Mkifichana mambo ya pesa mtaumiza uhusiano wenu.
KAZI ZA ZIADA
Haijalishi una hisia na makusudio mazuri sana, bila matendo yanayomridhisha mpenzi wako, hautaweza kujenga furaha ya kweli katika mahusiano yenu ikiwa utamficha mwenzi wako kuhusu kazi za ziada unazofanya. Ni muhimu pia kutambua kwamba pamoja na kuwa na makusudio na matendo mazuri, inakupasa kutilia mkazo kuwa matendo yako na makusudio yako yanaaminika kwa mpenzi wako kwa kumuambia ukweli.
Kama una kazi za ziada na ukawa unachelewa kurudi nyumbani, mwenzi wako anaweza kudhani kwamba ulikuwa na mchepuko, hivyo ukiwa na kazi za ziada, ni vema kumjulisha mwenza wako.
KUWA NA SIRI
Kuna mambo yanayopaswa kujulikana pande zote. Haipendezi ila ndio uhalisia kuwa pamoja na ukweli kwamba nyie mmeshibana katika mahusiano yenu, bado kutakuwepo na siri ambazo mwingine hapendi mwenzake ajuwe. Kufanya hivyo ni kuvuruga penzi lenu.
Mbaya zaidi katika siri hizo, inaweza kuwepo siri ya hisia halisi kuhusu upendo wa mpenzi wako kwako, au upendo wako kwake. Mfano, wapo waliooana lakini mmoja wao hasemi ukweli kama vile kama ana mtoto ambaye ameshazaa na mtu mwingine. Ili ujenge upendo katika ndoa ni vema jambo kama hilo kuliweka wazi mapema.
Ukweli mtu unapokuwa kwenye ndoa lazima mjenge mwenzako kwa kumuonesha kila kitu na kumthibitishia kwamba yule uliyezaa naye huna uhusiano naye tena, hapo utaonyesha kumjali mpenzi wako, hatimaye atajikuta anajiona unampenda kwa dhati.
KUKIRI KOSA NA KUOMBA MSAMAHA
Wapenzi ama wanandoa ni muhimu sana kuomba radhi unapojikuta umekosea. Kwa kawaida binadamu wengi hukumbuka mabaya kwa urahisi kuliko mazuri wanayofanyiwa. Na katika uhusiano, makosa haya mawili ; kwanza ni kudanganya na pili kutokuonyesha kujali unapokosea jambo, hudhoofisha uhusiano na kumvunja moyo mwenza wako.
Ni vema kukiri kosa kwa mwezako na kwa kufanya hivyo unamthibitishia kwamba kosa lile umelifanya kwa bahati mbaya. Inajulikana kwamba kuna makosa ambayo yanaweza kuwa makosa ambayo si rahisi kusahaulika, ingawaje mtu atajitahidi kusamehe na kujaribu kufanya uhusiano uendelee, jitahidi kumuonesha mwenzi wako kwamba hutarudia tena kosa hilo.