KAMWE, USILETE MAZOEA KWENYE NDOA
September 20, 2019
Edit
VIPO vitu vingi sana ambavyo kadiri unavyovifanya, ukavizoea, vinaleta tija lakini asikwambie mtu ndoa haihitaji mazoea.
Ndoa inatakiwa kuwa mpya kila siku. Kama ni kujifunza, kwenye ndoa unapaswa kujifunza kila wakati. Kila siku umuone mwenzi wako kama mpya vile, kama ndio kwanza mmeonana. Chukulia kama vile ndio umemuona kwa mara ya kwanza, unavyokuwa na kile ‘kiraruraru’ cha kumhitaji.
Nasema hivyo marafiki zangu kwa sababu mimi na wewe ni mashahidi katika hili. Tunashuhudia namna ambavyo matatizo mbalimbali yanatokea. Watu wanagombana, watu wanashitakiana kila kukicha, watu wanaachana.
Ukichunguza kwa makini, chanzo kikubwa cha watu kufikia hatua hiyo ni mazoea. Wameishi miaka mingi, wamezaa, wamezoeana kupita kiasi. Mke hana habari tena na mume. Mume naye ndio usiseme, hana muda na mke.
Wanachukuliana poapoa tu. Kinachotokea, kama zamani walikuwa wana tabia ya kujaliana kila wakati, inafika wakati wanaacha kabisa. Walikuwa wanapigiana simu kila wakati, inafika wakati hawapigiani hata siku mbili tatu.
Wanapigiana pale kunapokuwa na jambo la msingi tu. Mtoto anaumwa, ada inahitajika
haraka na mambo mengine yanayofanana na hayo. Zile za kuulizana ‘baby unakula nini leo’, ‘mpenzi nikuletee zawadi gani’ zinakoma kabisa.
Mume naye anakuwa bize na marafiki zake. Ndoa itawakutanisha jioni au usiku. Usiku wenyewe kila mtu akifika anakuwa na hamsini zake. Wanalala kama vile mtu na kaka dada yake.
Hiyo yote inaletwa na mazoea. Mke anamzoea mume wake hadi inafika wakati anapoteza hamu naye. Awepo sawa, asiwepo hewala, vivyo hivyo mume. Naye anamuona mke kama vile mtoto wa ba’mkubwa.
Nyumbani mke hana muda na mume. Akirudi mambo yote anamuachia dada wa kazi. Aandae maji ya kuoga, chakula na hata usafi wa chumbani kwao.
NI RAHISI KUTAMANI MTU MWINGINE
Kadiri mazoea yanavyozidi kushika hatamu, ni rahisi sana mke kumtamani kijana f’lani sharobaro kutokana na namna ambavyo anajua kujali hata kwa kuuliza vipi umeamkaje?
Hii haina tofauti na yule fundi ambaye anamwita na kutokea kwa wakati pale gari lake linapokuwa limeharibika barabarani. Gari kanunuliwa na mumewe lakini fundi anakuwa mwepesi sana kufika au kutoa msaada eneo la tukio kuliko mume.
Fundi anajali adha anayoipata mke wa mtu barabarani kuliko mwenye mke. Mwenye mke akipigiwa simu na mkewe kuambiwa kwamba gari imeharibika, anachukulia poa. Majibu ni yale ya ‘sasa mimi nifanyaje? Si umuite fundi?’ Hayo ndio mazoea yenyewe!
Mazoea yanasukuma hata suala la faragha liwe la kawaida tu. Liwepo lisiwepo yote heri. Wanaishi pamoja hata miezi miwili, hakuna anayemgusa mwenzake. Matokeo yake, atakazidiwa na matamanio na akapata mtu wa kumtamani, anampa nafasi.
Akimpata mtu anayejua kujali, anayejua ‘vurugu za mapenzi’ anashawishika. Anajikuta huko sababu tu ya mazoea mliyoyaweka. Usaliti unakua na hata kuhatarisha ndoa yenyewe.
ACHA MAZOEA
Mnapaswa kuishi hivyo miaka yote. Chukulia kama ni jukumu. Usiufanye uhusiano wako uchache. Kila siku uamshe kwa staili tofauti tofauti. Kama ulikuwa una tabia ya kumtoa ‘out’, zidisha kasi. Kama ulikuwa unamthamini kwa shida na raha basi hayo ndiyo yawe maisha yako.
Mpende, mdekeze ikibidi maana huyo ndio wako. Hakuna mwingine. Dekezaneni kila inapobidi maana hakuna namna. Kila mmoja awe na hamu na mwenzake kila wakati. Usichukulie poa, thamani ya mke au mume inapaswa kuwa vilevile kila siku.
Kila mmoja aguswe na maumivu ya mwenzake. Mkianguka kwenye shida muwe pamoja na mkiwa kwenye raha basi mfurahi pamoja. Heshimuni ndoa, iwekeni mbele na muipe thamani kila uchwao!
Mkiishi kwa staili hiyo, maisha mtayaona matamu na hakuna kitakachowayumbisha!