RAHA YA MCHEZO NI MAANDALIZI YA KISAIKOLOJIA SIYO UCHAWI
July 07, 2019
Edit
JUMAA ya leo ningependa tujadiliane jambo la tofauti kidogo! Kabla ya yote, tukubaliane kwamba usiri na kukosa uwazi kwenye mambo yahusuyo faragha, ni tatizo ambalo limesababisha uhusiano na ndoa nyingi kuvunjika.
Unakuta mtu ana tatizo kubwa kati yake na mwenzi wake, kwa sababu alishaaminishwa kwamba mambo haya ni siri na hayatakiwi kuzungumzwa popote, anabaki akiugulia ndani kwa ndani na mwisho uzalendo unapomshinda, anaamua kubwaga manyanga.
Wahenga walisema mficha maradhi, kifo humuumbua, usiwe miongoni mwa watu ambao wanaficha matatizo yao ya ndani, wakati mengine ni ya kawaida na yanatibika kwa urahisi! Maisha yamebadilika na sasa tunaishi kwenye zama nyingine kabisa, za ukweli na uwazi. Nimeanza hivyo kwa sababu nimekutana na visa kadhaa, vyote vikiwa vinafanana kutoka kwa watu wa rika mbalimbali.
Tatizo ambalo leo ningependa kulizungumzia, ni idadi kubwa ya wanandoa, hasa wanawake kulalamika kwamba wanapokuwa kwenye uwanja wa fundi seremala, wenzi wao hawawapi kile wanachokitarajia na matokeo yake, ile raha ya tendo la ndoa wamebaki kuisikia kwenye bomba. Tukubaliane kwamba ni kweli wanaume wengi siku hizi wana tatizo la nguvu za kiume na hilo nimeshalizungumzia mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na kupeana mbinu za namna ya kupambana na tatizo hilo.
Hata hivyo, itakuwa si sawa kuwa kila siku tunazungumzia upande mmoja tu, kwamba ikitokea mwanamke ameshindwa kufikia kilele cha raha katika tendo, basi lawama zinabaki kwa mwanaume! Upo ushahidi wa wanaume waliokamilika, kwa maana ya wasio na tatizo kabisa la nguvu wala maumbile lakini bado wenzi wao wanalalamika kwamba hawafurahii ngoma zaidi ya kuumia na kuchukia mchezo mzima.
Labda nizungumze kwa lugha nyepesi, wakati wanawake wengine wakilalamika kwamba wenzi wao wanawahi kwenye tendo na hawawapi raha wanayoitarajia, wapo wanawake wengine ambao wanalalamika kwamba wawapo kwenye tendo, hawafurahii chochote zaidi ya kusikia maumivu makali mpaka kufikia hatua ya kulichukia tendo.
Sasa ukizitazama pande hizi mbili, utagundua kwamba japokuwa suala la nguvu ni tatizo, bado lipo tatizo lingine kubwa ambalo ndiyo ningependa leo kulizungumzia. Tendo la ndoa linahusisha hisia na ili ulifurahie, ni lazima hisia zako ziwe zimetulia, usiwe na mawazo, usiwe na hofu, hasira, majuto wala chuki ndani ya moyo wako, yaani akili yako ifikiria jambo moja tu, raha ya mapenzi.
Hata hivyo, bahati mbaya ni kwamba si wote wanaoweza kutuliza akili zao wawapo kwenye tendo kwa sababu mbalimbali lakini kubwa ikiwa ni maandalizi kabla ya tendo. Upo ushahidi kwamba, hata kama ulikuwa na mawazo, hasira, chuki, kinyongo au hisia zozote mbaya kabla ya tendo, mwenzi wako akitumia muda wa kutosha kufanya maandalizi, hisia zote huyeyuka kama barafu juani na hatimaye kufikia utulivu wa kiakili.
Akili ikitulia, ndipo unapoweza kulifurahia tendo na pengine jitihada kidogo tu za mwenzi wako, zinaweza kukufanya uhisi kama unaimiliki dunia nzima. Kwa hiyo, jambo la msingi ambalo kila mmoja anapaswa kulizingatia, ni maandalizi ya kimwili, kiakili na kihisia kabla ya tendo.
Je, wewe unafahamu nini kuhusu maandalizi kabla ya kuingia uwanjani? Huwa unafanya kwa kiasi gani? Umewahi kuzungumza na mwenzi wako kuhusu mambo yenu ya faragha au ndiyo unaugulia ndani kwa ndani? Hebu tubadilishane mawazo kupitia namba za hapo juu na wiki ijayo tutahitimisha kwa kuelekezana nini cha kufanya ili kufurahia tendo.
Tukutane wiki ijayo.