AMEKUVUNJA MOYO WAKO NA KUKUACHA NA MAJONZI SOMA HAPA
July 04, 2019
Edit
MAUMIVU katika mapenzi huwa hayazoeleki. Hata kama unajifanya wewe ni shujaa kiasi gani, inapotokea yule unayempendaye akakuumiza, akauvunja moyo wako, akaondoka na kwenda mbali na wewe, lazima utaumia sana!
Maumivu ya kimapenzi yanakufanya ujihisi ni kama umekatwa mikono na miguu, unahisi kama dunia yote imefika mwisho, unaona kila kitu kibaya! Kama hujawahi kuyapitia, basi omba yasikukute.
Mara nyingi, wengine inapotokea wameumizwa na wale waliokuwa wanawapenda sana, hufikiria kujidhuru kwa kujinyonga, kunywa sumu au kujipiga risasi! Wengine huamua kuwadhuru wale waliowakataa!
Wengine hujikuta wakitopea kwenye matumizi ya madawa ya kulevya, pombe au tabia nyingine hatarishi kama kujihusisha na ngono zembe na watu tofautitofauti, wakiamini eti ndiyo wanapunguza machungu. Huko kote ni kujidanganya na kuongeza matatizo.
Ikitokea amekuumiza moyo wake na kukuacha, tambua kwamba maumivu unayoyapitia ni ya muda tu! Utaumia sana, utateseka sana ndani ya moyo wako, utalia na kusaga meno lakini hayo yote ni ya kupita. Zifuatazo ni mbinu zitakazokusaidia unapopitia katika kipindi kama hiki.
OMBOLEZA, KUTOA MACHOZI NI DAWA
Maombolezo siyo lazima uwe umepatwa na msiba tu, unapokutana na tukio la kuumiza moyo wako kwa kiasi hiki, jipe nafasi ya kuomboleza. Chukulia kama yule mtu aliyekuumiza amefariki dunia na hutamuona tena maishani mwako.
Jipe muda wa kuwa peke yako na zungumza na moyo wako. Lia, toa machozi, huzunika! Hakuna ubaya wowote wa kulia. Wengine hudhani kwamba kwa kujikaza wasitoe machozi basi wanaonesha uimara wao. Hapana, acha moyo utoe maumivu yote yaliyomo ndani yake.
Zungumza na watu wako wa karibu, washirikishe, waeleze jinsi unavyojisikia. Kama unao uwezo, mtafute mshauri wa saikolojia atakusaidia kukuonesha njia.
JIJALI, WEWE NI MUHIMU ZAIDI
Kama nilivyosema, baadhi ya watu wanapoumizwa, hufikia hatua ya kujidhuru au hata kuyakatisha maisha yao, au kuingia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya na pombe. Watu wa namna hii, wanakuwa hawaijui thamani yao wala hawajui kwa nini wameletwa duniani.
Hebu jiambie mara kwa mara kauli hii ‘mimi ni muhimu kuliko mtu mwingine’. Ndiyo, ulimpenda sana, yeye ndiyo alikuwa kila kitu kwako na mlipanga mambo mengi lakini unatambua kwamba wewe ni muhimu zaidi kuliko yeye? Kama ulikuwa hujui, ndiyo nakwambia sasa, wewe ni muhimu kuliko mtu yeyote chini ya jua.
Akikuacha, wala usijione huna thamani! Jifanyie mambo mazuri, toka ‘out’ peke yako, nenda sehemu nzuri itakayokusahaulisha machungu uliyonayo, jinunulie zawadi nzuri, kula vyakula vizuri, pata muda wa kufanya mazoezi na jipumzishe. Jifanyie mambo mazuri kwa sababu wewe ni wa thamani.
Hakikisha kila siku unapendeza, isiwe kwa sababu amekuacha basi huoni hata umuhimu wa kuoga, kuvaa nguo safi na kupendeza! Wewe ni wa muhimu zaidi.
JIWEKE BIZE
Kama wewe ni mfanyakazi, basi elekeza nguvu na akili zako zote kwenye kazi, kama ni mwanafunzi pia elekeza nguvu zako kwenye masomo. Mwanzo unaweza kukumbana na ugumu kwa sababu kichwa chako kinakuwa na mambo mengi lakini jilazimishe! Unapoiweka akili yako na mwili wako bize, unapunguza ule muda wa hisia mbaya kukuumiza.
Usikae na kujiinamia, ukiwa umejishika tama! Jichanganye na wenzako, kama muda wa kazi umeisha, nenda kafanye mazoezi, kama huwa unapenda kuimba au kucheza, jichanganye na taratibu utaanza kuona tofauti.
Itaendelea wiki ijayo.