SIMULIZI YA MFALME NA MBWA WAKE 10
June 15, 2019
Edit
Kulikuwa na mfalme mmoja aliyekuwa na mbwa kumi wakali sana. Alipenda kuwatumia mbwa hawa pindi akitaka kumuadhibu mtumwa aliyekosea.
Mbwa hawa waliwatesa watumwa kwa kuwararua na meno yao makali! Wakati mwingine watumwa waliokutana na adhabu hii walipoteza uhai.
Siku moja mtumwa aliyemtumikia mfalme kwa miaka kumi alitoa wazo baya ambalo halikumpendeza mfalme, ikaamriwa akamatwe na kutupwa katika banda la mbwa.
Mtumwa alinung'unika na kusema :"nimekutumikia kwa miaka 10, na leo wanitenda hivi? Naomba unipe walau siku 10 kabla hujanitupa bandani! " Mfalme akakubali.
Katika siku hizo 10, mtumwa alimfuata mlinzi wa banda la mbwa na kumuomba ampe nafasi ya kuwahudumia mbwa wale. Mlinzi alistaajabu ila akakubali. Mara moja mtumwa akaanza kazi ya kuwapa mbwa chakula, kuwaogesha na kila aina ya faraja ambazo wanyama huhitaji.
Siku 10 zikaisha, mfalme akaamuru mtumwa atupwe bandani kutumikia adhabu yake.
Hilo likafanyika kwa haraka, lakini cha kushangaza mbwa walianza kulamba miguu ya mtumwa na si kumrarua kama ilivyotegemewa. Mfalme akastaajabu, akasema:"Nini kimewasibu mbwa wangu? ",.
Mtumwa akajibu :" nimewahudumia mbwa hawa kwa siku 10 tu na hawajasahau fadhila zangu.
Lakini kwa upande wako nimekutumikia miaka 10, hata hivyo umesahau yote kwa sababu ya kosa moja tu! " Kufikia hapo mfalme akatambua kosa lake na akaamuru mtumwa aachiwe huru.
Katika maisha kuna watu husahau mambo mema waliyotendewa na wengine pindi wakikosewa.
Kamwe usiruhusu historia nzuri kufutika sababu ya jambo moja usilolipenda! Tembea katika
msamaha kila wakati.Mungu Awabariki wote.