Hatua 5 za kuzungumza na mpenzi wako aliyekasirika - RAHA ZA KITANDANI

Hatua 5 za kuzungumza na mpenzi wako aliyekasirika


Kwenye mapenzi kuna nyakati za kutofautiana, kukasirishana. Katika hali ya kawada kipindi hiki huwa ni za hatari kwa sababu husababisha nyufa kubwa za uhusiano na kulifanya penzi kukosa ladha.

Sote tunajua, watu hupigana, huachana, hujeruhiana, hutukanana, hudhalilishana wakiwa na hasira. Hata hivyo si wote wanaojua wafanye nini wanapojikuta wameingia kwenye hatua hiyo mbaya.

Msomaji wangu, hebu jaribu kukumbuka ugomvi mmoja uliotokea kati yako na mpenzi wako na ikiwezekana jikumbushe mlivyoanza! Utabaini kuwa mlianza kama utani na mkajikuta mmefura kwa hasira, mkatwangana makonde, mkatamkiana maneno makali ya kuudhi na pengine mkaamua kuachana.

Yote hii ni kwa sababu mlikosa elimu ya mazungumzo. Ingekuwa mmoja wenu hasa yule aliyekuwa wa pili kukasirika anafahamu hatua za kuzungumza na mtu aliyekasirika angechukua jukumu la kutuliza machafuko na kuleta amani kwenye mapenzi. Tazama hatua tano za kuzungumza na mpenzi aliyekasirika.

MPUNGUZE MHEMKO
Hasira hujaza kifua, huathiri mzunguko wa damu na ufahamu. Mtu aliyekasirika huwa vigumu kwake kusikiliza au kutazama mambo kwa jicho la tatu. Mwenye hasira huwa hafikirii matokea yajayo badala yake hutazama zaidi tukio na jinsi ya kupata ushindi iwe kwa maneno au kwa mapambano.

Katika hali ya namna hiyo, mtu mwingine akija na busara za kutaka kumgeuza haraka haraka hawezi kumuelewa. Muhimu hapo ni kuacha kumwadama, kujibizana naye, kumshawishi asikilize badala yake mpe nafasi ya kusema atakavyo, abwate ajuavyo huku wewe ukimuitikia na kumkubalia lawama zake. “Basi mpenzi mwenye makosa ni mimi.” Kauli za aina hii zitampunguza hasira kwani atajiona msindi.

MSOME SAIKOLOJIA YAKE
Kwa kuwa unamfahamu mpenzi wako kwa kina itakuwa rahisi kwako kumtambua kuwa amepunguza hasira na kurudi katika hali yake ya kawaida. Ukisha fahamu hilo chukua jukumu la kumsoma kisaikojia ili kujua kama yuko kwenye hali nzuri ya kusikiliza yale uliyotaka kumwambia wakati alipokuwa na hasira.

Zoezi hili linaweza kuchukua saa kadhaa na wakati mwingine hata siku mbili. Lengo ni nini? Ni kupata matokeo sahihi ya kuondoa chuki za mwenza wako na kumfundisha madhara ya kukasirika kwenye uhusiano wenu wa kimapenzi. “J, nakupenda sana, lakini juzi uliniumiza, uliniambia mimi malaya kwa kosa ambalo sikufanya?” Bila shaka muda huo atakusikiliza zaidi kuliko ungebishana naye alipokuwa na hasira.

MRUHUSU AKUJIBU
Pamoja na kumsoma kisaikojia na kumwambia kinagaubaga makosa yake, usimzuie kujitetea, mpe nafasi ya kuzungumzia kilichomkasirisha. “Unaona bado unanitukana, sasa naamini siku ile ulikuwa umedhamilia.” Usisiseme hivyo, mwache ajibu hoja hata kama atakuwa anakukandamiza na kuzidi kujijengea ushindi. Mvumilie aoshe ubongo wake.

EPUKA MARUMBANO
Kama nilivyosema kwenye hapo juu, wapenzi wengine huwa wagumu kuelewa, ni watu wa kuficha udhaifu wao na kutopenda kuonekana wamekosea. Watu wa namna hii unapowarejeshea mazungumzo wanaweza kujikuta wanahamaki tena.
“Kwa hiyo ulikuwa unasemaje…nilifanya ndiyo,… wewe unaamuaje?” Mkifika kwenye alama hiyo usikubali kurumabana naye mwache aseme halafu wewe ingia kwenye hatua ya tano.

MUOMBE MSAMAHA
Hata kama atakuwa yeye ndiye mwenye makosa na amekataa kukiri, usijali, chukua jukumu la kumuomba msamaha na kueleza tena nia yako ya kumazungumzo ilikuwa ni kuelewana si kugombana. Kumbuka hata kama amekiri kosa, bado unatakiwa kumuomba radhi kwa kurejea yaliyopita. “Mpenzi inawezekana nikawa nimekuudhi kwa niliyosema, nakuomba sana tusameheane.”

Bila shaka kwa haya machache msomaji wangu utakuwa umejifunza na kuchukua hatua za kuzuia migogoro mikubwa inayotokana na hasira za mpenzi wako. Leo niishie hapa, nikushukuu kwa kunisoma. Kaa mkao wa kura, kile kitabu bora cha mapenzi nchini TITANIC, TOLEO LA NNE, kitakuwa mtaani hivi karibuni. Usikose nakala yako.