TABIA HIZI ZINAPUNGUZA HISIA ZA UPENDO KWA MWENZAKO - RAHA ZA KITANDANI

TABIA HIZI ZINAPUNGUZA HISIA ZA UPENDO KWA MWENZAKO

UNAISHI vipi na mwenzako? Namna unavyoishi naye kuna mchango mkubwa sana ima wa kuongeza ama kupunguza kiwango chake cha upendo kwako.
Kama ambavyo nimewahi kusema, kitendo cha kupendwa si kazi sana ila kazi nzito ni kufanya anayekupenda leo aendelee kukupenda kila siku. Hapa ndipo kwenye mtihani na vijana wengi wameshindwa.
Tathmini inaonesha wengi huingia katika uhusiano wakiwa wanapendana ila aina ya tabia zao ndiyo huwa chachu ya kupoozesha nguvu ya upendo ambayo huwapo baina yao na hatimaye kuimaliza kabisa.
Ingawa kuna tabia nyingi zinazopoozesha nguvu ya upendo na hatimaye kuimaliza kabisa, leo nimeamua kuchambua tabia chache ili iwe chachu ya watu wenye tabia hizi kufanya mabadiliko mapema.
  1. KUWABANA SANA WENZAO
Hili wengi huwa hawalifahamu. Wengi wanajua kwenda na wapenzi wao jino kwa jino (kuwabana mno) ndiyo njia mwafaka ya kuwafanya wawapende. Sio kweli hata kidogo.
Mapenzi ni hisia. Na hisia ili iweze kuwa na nguvu juu ya mhusika ni lazima utoe nafasi ya kufikiri (imagination) kwa mhusika. Sasa unapombana sana mwenzako, unamnyima nafasi ya kukaa na kukumis hivyo anakosa fursa ya yeye kuanza kukufikiria vema na kukujaza katika akili na hisia zake ipasavyo.
Unapohakikisha mwenzako anakupenda na umemfanyia matendo mengi mema ya kumtia furaha na uwendawazimu, toa nafasi kwake ya kukumis. Si kila wakati uko busy kukagua simu yake tu. Sio kila wakati unakaa na kumzuia hata kutoka nje. Unakosea.
Mwenzako ili akupende sana inabidi apate muda wa kumisi matendo yako na kukufikiria. Na kadiri atakavyokuwa akikufikiria ndivyo anazidi kukuweka katika akili yake na kuwa ngumu yeye kuamini kuna maisha bila wewe.
Kumbuka japo wivu ni moja ya alama za upenndo ila ukikithiri ni karaha kwa mwenzako na shida kwako katika maisha. Kama unahisi una tatizo la wivu uliokithitri, ona watalaamu haraka ili uwezo kuishi maisha ya amani huku ukidumisha furaha ya uhusiano wako.
  1. KUDHARAU NDUGU ZAKE
Japo mapenzi ni suala linalowahusu sana wewe na mwenzako, ila ili uhusiano wenu uwe na ladha na mwenzako ajione mshindi kuwa na wewe, basi hakikisha unawaheshimu na kuwajali nduguze.
Kuwajali ndugu zake maana yake kutowaongelea vibaya na kuwatendea wema kwenye kila fursa unayotakiwa kufanya hivyo.
Ukijifanya mjanja eti kuwadharau ndugu zake mpaka yeye akajua kwa kigezo kwamba wewe unapendana naye hivyo wao hawakuhusu, utakuwa unakosea sana.
Kumbuka yeye na ndugu zake wamekuwa pamoja pengine toka utoto, wamekula pamoja, wamecheza pamoja na wameishi katika mazingira yanayofanana kwa muda mrefu. Kwa sababu hii, hawa wana muunganiko imara sana (strong bond), usitegemee sana yeye kuwadharau ndugu zake kisa wewe kwa kigezo cha upendo.
Anaweza kuvumilia kero na maudhi ya mara kwa mara unayowafanyia ndugu zake ila ukweli ni kwamba kadiri utakavyokuwa unawafanyia yasistahili ndivyo kiasi cha upendo wake juu yako pia kitakavyokuwa kinayeyuka.
Kitayeyuka kwa sababu kuu mbili, kwamba hatokuwa akifurahia ndugu zake wakifanyiwa ujinga ila pia lawama halisi za ndugu zake juu yako zitamfanya ajihisi ‘muasi’ kwa kuendelea kuwa na wewe ambaye unawatia unyonge ndugu zake.
  1. KUMTISHIA KUMUACHA
Wapo wengi wenye tabia hii. Wakikerwa na wenzao ama kukitokea kutoelewana wanakimbilia kusema tuachane ama nitakupa talaka. Ingawa wengi wenye kusema kauli hii huwa wanasukumwa na hasira dhidi ya kero waliyofanyiwa na wenzao ila kitu hiki si kizuri hata kidogo.
Binadamu ni kiumbe wa tahadhari sana, kila anapohisi kuna hatari ama kuachwa hujiandaa. Hivyo wakati wewe unasema kwa hasira tuachane mwenzako anapata tafsiri kwamba huhofii kumpoteza hivyo kujiona hayuko salama sana kuwa na wewe.
Kwa maana hiyo, bila wewe kujua anawenza kuanzisha mahusiano mapya na mwingine ama kuanza kuamini kwamba wewe huna mapenzi ya dhati juu yake, vyote hivi vina athari kubwa katika upendo wenu kwa sababu vitamfanya asikufikirie tena katika uzito mkubwa kama ilivyokuwa hapo awali.
Kuwa makini sana na kauli hii ya tuachane. Japo unaweza kuichukulia kawaida ila inaweka sumu katika ustawi wa mahusiano yenu.
  1. USITHUBUTU KUMFANYA AJIHISI MNYONGE
Hakuna  ambaye anapenda kuwa na mtu ambaye kupitia kauli na matendo yake yatamfanya ajihisi mjinga, dhaifu na asiye na maarifa.
Kila mmoja anaingia katika mahusiano ya kimapenzi mbali na mambo mengine ila ni kuwa na mtu atakayemfanya ajihisi imara na mwenye kusitirika.
Usipende kuongea hovyo mambo ya kijinga ya mpenzi wako kwa watu wasiostahili. Kama unataka kupata ushauri ama kupunguza machungu yako, basi tafuta mtu makini wa kuzungumza naye.
Mwenzako akisikia aibu yake imesambaa mtaani mbali na mambo mengine, ila  ataona unamdhalilisha bila hata kufikiria ujinga anaofanya ama anaokufanyia.
Wanawake wengine  wenzao wakiwa wanapitia changamoto ima ya kimaradhi ama kazi basi wao ndiyo wanakuwa vinara wa kusambaza habari hizo mtaani. Kufanya hivyo ni ujinga.
Kuwa stara kwa mwenzako kwa sababu hicho ndiyo kitu anachotaraji mno. Instgram: ramadhani.masenga
Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia (Psychoanalyst)